Fahamu Faida za Kiafya za Kitunguu Swaumu (Garlic)
Kitunguu swaumu ni jamii ya vitunguu ambayo kwa kitaalamu huitwa Allium sativum.
Jamii hii ilianza kutumika katika mabara mbalimbali duniani hususani
Asia, Afrika na Ulaya takribani miaka 6000 iliyopita. Matumizi makuu
nyakati hizo yakiwa viungo katika mboga na tiba.
Kitunguu
swaumu kimetajwa kwenye vitabu mbalimbali vya dini vikielezea faida
zake katika kutibu maradhi mbalimbali yasababishwayo na bakteria,
matatizo katika mapafu, matatizo katika mfumo wa umen'genyaji chakula,
na matatizo ya kuishiwa nguvu.
Historia
inaonesha kuwa, vitunguu swaumu vilianza kutumika China mwaka 510 K.K
na pia vilitumiwa na wanajeshi wa Ugiriki na Roma. Aidha wasafiri wa
vyombo vya baharini na vijijini pamoja na wakulima barani Afrika
walivitumia sana.
Mwaka
1858, mtafiti na mwanasayansi wa nyakati hizo, Louis Pasteur aligundua
uwezo wa kitunguu swaumu katika kuua vimelea mbalimbali vinavyosababisha
magonjwa, na hivyo vikaanza kutumika kama dawa ya kusafishia vidonda na
kuzuia kidonda ndugu hasa zama za vita ya kwanza na pili ya dunia.
Isitoshe, mpaka sasa zipo dawa kadhaa zilizotengenewa kwa kutumia jamii
hii ya vitunguu swaumu ikiwemo dawa ya kusafisha mdomo (mouth wash)
ingawa watumaiji wake wengi huilalamikia dawa hiyo kwa sababu ya harufu
mbaya ya dawa hiyo inayowasababishia kunuka kwa mdomo.
Faida za vitunguu swaumu
Katika
tafiti mbalimbali vitunguu swaumu vimeonekana kuwa na uwezo wa kutibu
maambukizi ya bakteria, fangasi na virusi vya aina mbalimbali. Aidha
husaidia kuzuia magonjwa ya moyo ikiwemo kuondoa lijamu katika mishipa
ya damu na hivyo kusaidia katika kurekebisha shinikizo la damu. Faida
nyingine za vitunguu swaumu ni pamoja na
- Kutibu saratani ikiwemo saratani ya tumbo na utumbo mkubwa. Tafiti zinaonesha idadi ndogo ya wagonjwa wa saratani katika nchi ambazo wakazi wake wana utamaduni wa kutumia vitunguu swaumu kwa wingi.
- Vitunguu swaumu husaidia kudhibiti kiwango cha sukari katika damu. Hata hivyo inashauriwa kwamba wagonjwa wa kisukari wanaotumia sindano za insulin wasitumie kitunguu swaumu kwa wingi mpaka watakaposhauriwa na daktari.
- Huzuia kusanyiko la chembe sahani zinazosaidia kuganda kwa damu (platelet aggregation)
- Husaidia ufyozwaji wa thiamin, hivyo kusaidia kuepusha mwili na ugonjwa wa beriberi
- Ina kiasi kikubwa cha vitamini C ambayo husaidia kuzuia ugonjwa wa kiseyeye
- Hutumika kutibu magonjwa nyemelezi kama toxoplasmosis, hasa kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini.
Ushahidi wa Kitafiti
Katika
utafiti uliofanyika nchini Czech ilionekana kuwa matumizi ya vitunguu
swaumu yalisaidia sana katika kupunguza kusanyiko la lijamu
(cholesterol) pamoja na mafuta yasiyofaa mwilini (low density
lipoproteins) katika mishipa ya damu. Aidha, mwaka 2007 BBC iliripoti
matumizi ya vitunguu swaumu katika kusaidia kumkinga mtumiaji dhidi ya
aina fulani ya mafua iliyosababishwa na virusi. Mwaka 2010, ulifanyika
utafiti mwingine ambao ulijumuisha wagonjwa 50 wenye shinikizo la damu
sugu ambalo lilikuwa ni vigumu kudhibitiwa hata kwa matibabu
yaliyozoeleka ya dawa na njia nyingine. Kama njia ya kuchunguza ufanisi
wa vitunguu swaumu katika kutibu shinikizo la damu, baadhi ya wagonjwa
hao walipewa vitunguu swaumu wakati wengine walipewa dawa isiyohusika na
matibabu ya shinikizo la damu (au placebo). Ilionekana kuwa wale
waliopewa vitunguu swaumu kama dawa ya shinikizo la damu walionesha
maendeleo mazuri kwa vitunguu swaumu kuweza kushusha vizuri kiwango cha
shinikizo la damu, hususani systolic pressure, tofauti na wale waliopewa
placebo.
Nini siri ya kitunguu swaumu?
Sifa
kuu zinazokifanya kitunguu swaumu kuwa na uwezo na faida zilizoainishwa
hapo juu ni kule kuwa kwake na viasili kadhaa (ingredients) ambavyo
vinafanya kazi tofauti tofauti. Uwezo wake wa kiutendaji unatokana na
mambo yafuatayo;
- Vina uwezo wa kusababisha kutanuka kwa mishipa ya damu (vasodilation) kwa kubadilisha polysulfides zilizopo ndani yake kuwa hydrogen sulfides kwenye seli nyekundu za damu.
- Husaidia uthibiti wa kiwango cha sukari mwilini kwa kushusha kiwango cha kemikali ya homocystine na kupunguza madhara ya kisukari.
- Iwapo vitapondwa pondwa vizuri, vitunguu swaumu hutoa kemikali iitwayo Allicin ambayo ni dawa dhidi ya bateria, na phytoncide ambayo huua fangasi wa aina mbalimbali.
- Harufu mbaya ya kitunguuu swaumu hutokana na gesi aina ya hydrogen sulfide ambayo inayotolewa baada ya kuvila.
Nini Madhara ya vitunguu swaumu?
Ukiacha faida zake, vitunguu swaumu pia vina hasara na madhara mbalimbali kwa mtumiaji. Madhara hayo ni pamoja na;
- Harufu mbaya mdomoni ambayo hutokana na kemikali ya AMS (allyl methyl sulfide). Harufu mbaya hii, hata hivyo, yaweza kupunguzwa kwa kunywa maziwa au kunywa maji mengi.
- Kwa baadhi ya watumiaji, vinaweza kuwaletea mzio au mcharuko mwili (allergies au inflammatory reactions)
- Kichefuchefu, Kutapika na kuharisha.
- Huweza kusababisha hatari ya kuvuja damu, kwa sababu huzuia kazi ya seli sahani (platelets) zenye kusaidia kuganda kwa damu kushindwa kufanya kazi yake vizuri, na hususani kwa mama wajawazito, baada ya upasuaji au mara baada ya kujifungua.
- Huingiliana katika utendaji kazi wake na dawa kadhaa kama vile warfarin, antiplatelets, saquinavir, dawa za shinikizo la damu kwa ujumla hasa calcium channel blockers, na antibiotiki za jamii ya quinolone kama vile ciproflaxacillin.
- Aidha, vinaelezwa pia kuwa na madhara kwa wanyama jamii ya paka na mbwa
No comments:
Post a Comment