SERIKALI imesitisha wimbo na video ya ‘Chura’ wa msanii, Snura Mushi
‘Snura Majanga’, kuchezwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari hadi
itakapofanyiwa marekebisho. Wimbo na video hiyo umetokana na maudhui ya utengenezwaji wake ambayo hayaendani na maadili ya Mtanzania.
Pia Serikali imesitisha maonyesho yote ya hadhara ya msanii huyo,
mpaka atakapokamilisha taratibu za usajili wa kazi zake za sanaa katika
Baraza la Sanaa la Taifa (Basata). Licha ya hivyo, Serikali imewataka wasanii wajiulize kabla ya kubuni
kazi zao za sanaa kwa kufikiria wazazi, ndugu, jamaa na marafiki zao
namna watakavyozipokea.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Zawadi Msalla,
aliwaambia waandishi wa habari kwamba wasanii wanapotunga nyimbo zao
wavae nafasi za wanaowadhalilisha na waelewe kwamba sanaa si uwanja wa
kudhalilisha watu.
“Serikali imechukizwa na kazi hiyo ya Snura kwa kuwa si tu
inadhalilisha tasnia ya muziki, bali inadhalilisha utu wa mwanamke kiasi
kwamba jamii inaanza kuhoji hadhi ya msanii, weledi na taaluma ya sanaa
kwa ujumla,” alieleza Msalla.
Msalla aliongeza kwa kuwataka wananchi kutojiingiza katika makosa ya
sheria ya mtandao, kwa kusambaza wimbo huo kwa njia yoyote ya kimtandao. Pia alivitaka vyombo vya habari viwe vya kwanza kuchuja maudhui ya
kazi za sanaa, kabla ya kuwa mawakala wa uharibifu wa jamii kupitia
kucheza kazi chafu za sanaa.
Hata hivyo, inadaiwa baada ya Snura kuitwa na Wizara ya Habari,
Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa ajili ya utetezi wake alishindwa
kujieleza alipotakiwa kueleza anajisikiaje kumdhalilisha mwanamke wakati
yeye ni mwanamke. Inadaiwa Snura alikosa la kujibu zaidi ya kuomba msamaha kwa Serikali imsamehe kwa alichokifanya.
Snura alipotakiwa na Mtanzania kuelezea alivyopokea kifungo hicho,
alidai kwamba atazungumza na waandishi wa habari leo katika mkutano
wake. “Leo (jana) sizungumzi chochote na waandishi nitazungumza kesho (leo)
katika mkutano wangu pale Idara ya Habari Maelezo nitatoa yangu,”
alieleza Snura.
Kabla wimbo huo haujatoka, Snura alikuwa akipiga picha za vipande
vikimuonyesha akiwa maeneo mbalimbali akitikisa umbo lake akimuwakilisha
chura. Baadhi ya vipande hivyo alivionyesha kama chura akiwa anafua,
anapika, anaumwa ametundikiwa dripu na nyinginezo jambo ambalo lilizua
maswali mengi ya kuhusu maadili ya Mtanzania kwa mashabiki wake na wadau
wa muziki kwa ujumla.
Wimbo wa video hiyo inakuwa ya pili kwa msanii huyo kufungiwa
kutokana na maadili mabovu, ambapo awali video ya Snura ‘Majanga’
ulifungiwa na kutolewa katika kinyang’anyiro cha vipengele vya kugombea
tuzo za muziki za Kili huku mwenyewe akilalamika kutotendewa haki.
Pamoja na wimbo huo, wimbo mwingine uliotolewa katika mchakato huo na
kufungiwa pamoja na ‘Majanga’ ni video ya wimbo wa ‘Uzuri wako’ ya
msanii, Juma Jux.
Nyimbo nyingine zilizowahi kufungiwa kutokana na kukiuka maadili ya
Mtanzania ni ‘Zigo’ wa Ambwene Yessaya ‘AY’ aliomshirikisha Diamond
Platinumz wa ‘Zigo’.
No comments:
Post a Comment